Friday, July 13, 2012

Simba na Yanga kupambana Canada

Majira ya joto ughaibuni,almaarufu kama summer huwa yana matukio mbalimbali yenye kuvutia na yenye lengo la kuwaunganisha wananchi na hususani watanzania wanaoishi katika nchi mbalimbali ulimwenguni. Miongoni mwa matukio ya namna hiyo, ni pamoja na michezo.
Katika kuendeleza “jadi” hiyo ya kujidai na kujumuika kunako majira ya joto, jiji la Toronto nchini Canada linatarajiwa kushuhudia mpambano wa kukata na shoka baina ya mashabiki wa Yanga na Simba wanaoishi nchini Canada. Pambano  hilo ambalo ni la marudiano linatarajiwa kufanyika Jumamosi hii tarehe 14 Julai katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Bur Oak uliopo katika mji wa Markham,Ontario ambao ni mji shirikishi wa eneo linalojulikana kama Greater Toronto Area(GTA)
Katika pambano la kwanza,mashabiki wa Yanga waliondoka vichwa chini baada ya kuangukia pua kwa kuchabangwa jumla ya magoli 8-3. Kutokana na kipigo hicho,Yanga wanasema ni muhimu kwao kulipiza kisasi na kulinda heshima ya Yanga. Tayari Yanga wameongeza nguvu kwa kuwaingiza kundini vijana sita ambao wapo chini ya umri wa miaka 20 kwa minajili hiyo hiyo ya kulinda heshima.
Kwa upande wa Simba,wao wanasema kama ilivyo jadi,ushindi kwao ni lazima na Yanga watarajie kipigo kingine kikali tu.
Waandaji wa pambano hilo wanaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuunga mkono timu zao wanazoshabikia. Mechi itachezeshwa na refa kutoka Iran ili kuondoa uwezekano wa “mlungula” na upendeleo.